Marekani
 imepinga hatua ya Urusi ya kuiondolea vikwazo vya silaha Iran, huku 
Urusi ikilenga kuipatia nchi hiyo mfumo wa kudhibiti makombora 
ujulikanao kama S-300.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John 
Kerry alimpigia simu waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, ambaye 
amesema uamuzi wa hiyari uliochukuliwa na Urusi kuiwekea vikwazo vya 
silaha Iran mwaka 2010 hauhitajiki tena, kufuatia muundo wa makubaliano 
wa kimataifa wa mwezi uliopita kuhusu mpango wa Iran wa nyuklia.Marekani inachukulia vikwazo hivi kuwa sehemu ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa ambavyo havitakiwi kuondolewa hadi mwishoni mwa mwezi Juni wakati mkataba wa mwisho utakapofikiwa.
Waziri wa Ulinzi wa Iran, Hossein Dehghan amesema uamuzi wa Urusi utasaidia kuanzisha usalama na utulivu katika eneo hilo. Lakini Israel imekosoa hatua hiyo.
Waandishi wa habari wanasema Israel inahofia kuwa mfumo wa kudhibiti makombora wa S-300 utafanya mashambulio ya anga dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran kuwa magumu zaidi.
