Mahakama ya Jinai mjini Cairo Misri, leo inatarajiwa kuendelea kusikiliza kesi ya rais wa zamani Muhammad Morsi ambaye alichaguliwa na wananchi na kupinduliwa na jeshi la nchi hiyo.
Televisheni ya Press TV imeinukuu
mahakama hiyo ikitangaza jana kuwa tarehe ya kusikilizwa kesi ya
Muhammad Morsi na wanachama wengine 10 wa Ikhwanul Muslimin imesogezwa
mbele hadi leo, Machi 26.
Muhammad Morsi na wanachama 10 wa
Ikhwanul Muslimin wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za ujasusi
na kulipatia nyaraka za siri shirika la kijasusi la Qatar na televisheni
ya al Jazeera ya Qatar.
Nyaraka hizo za siri za Misri ambazo
inadaiwa Morsi aliipatia Qatar ni pamoja na taarifa za siri kuhusu
jeshi la Misri na taarifa za siri kuhusu siasa za ndani na za kimataifa
za Misri.
Kuna uwezekano watuhumiwa hao wakahukumiwa adhabu ya kifo kama watapatikana na hatia.