ASKOFU MALASUSA akemea mauaji ya ALBINO nchini


ASKOFU MALASUSA akemea mauaji ya ALBINO nchini
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-KKKT, ASKOFU DOKTA ALEX MALASUSA, amekemea na kulaani matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi-ALBINO yanayotokea katika baadhi ya mikoa hapa nchini kwa kuwa ni kinyume cha haki za binaadamu na chukizo mbele za MUNGU.

ASKOFU MALASUSA amesema hayo Mjini BABATI mkoani MANYARA, wakati wa Ibada maalumu ya uchangishaji na kuweka Jiwe Kuu la Pembe la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa BABATI ambapo amewaomba wananchi kudumu katika ibada ili kujiepusha na maovu mbalimbali.

Askofu Malasula amesema vitendo vya kutoa uhai wa watu wenye Albinism havikubaliki. Amegusia pia matukio ya uvunjifu wa amani unaotokana na migogoro ya ardhi mkoani Manyara na sehemu nyingine nchini huku akiwanyooshea kidole watumishi wa serikali waliopewa dhamana ya kusimamia haki kutofanyakazi yao ipasavyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati wa Kanisa hilo, ASKOFU SOLOMON MASSANGWA ameitaka jamii kulinda amani na utulivu vilivyopo hapa nchini.

Akitoa salaam za serikali katika ibada hiyo, Mkuu wa mkoa wa MANYARA, DOKTA JOEL BENDERA, ameitaka jamii mkoani humo kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoutia doa mkoa huo ikiwemo mauaji, uharibifu wa mali vinavyotokana na migogoro ya ardhi.

Taarifa ya ujenzi wa Kanisa hilo iliyosomwa na WILFRED MUSHI imeeleza kuwa jengo hilo la kanisa lenye uwezo wa kukalisha watu elfu tatu kwa wakati mmoja, litagharimu shilingi Bilioni moja na milioni mia 2 hadi litakapo kamilika .

Post a Comment

http://www.princetarique.blogspot.com

أحدث أقدم

Comments System

blogger/disqus/facebook

Disqus Shortname

designcart