Tume ya uchaguzi nchini Nigeria imeahirisha uchaguzi mkuu ambao ulikuwa
ufanyike tarehe 14 mwezi huu kutokana na sababu za kiusalama....>>>
Uchaguzi huo sasa utafanyika tarehe 28 mwezi Machi.
Mkuu wa tume hiyo Attahiru Jega alisema kuwa amejulishwa na maafisa wa usalama kuwa wanajeshi hawatakuwepo kulinda vituo vya kupigia kura kwa kuwa watakuwa wakipigana na wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi.
Awali tume hiyo ilikuwa imetangaza kuwa haingewezekana kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura katika maeneo ambapo maelfu ya watu tayari walikuwa wamehama.
Mwandishi wa BBC anasema kuwa kuahrishwa kwa uchaguzi kutaleta utata kwa kuwa chama kikuu cha upinzani kimekashifu jeshi kwa kulazimisha kuahirishwa kwa uchaguzi huo ili kumsaidia rais Goodluck Jonathan kufanya kampeni.