Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (pichani), ametangaza maandamano na migomo isiyokoma nchi nzima ku
shinikiza kuvunjwa Bunge Maalumu la Katiba, kwa madai kwamba limekuwa likitafuna fedha za umma huku wakijua kwamba Katiba haiwezi kupatikana.
Alitangaza hilo wakati akihutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema unaoendelea jijini Dar es Salaam jana uliojumuisha zaidi ya wajumbe 922 kati ya 1,049.
Wajumbe wa mkutano huo walitarajiwa kumchagua Mwenyekiti na viongozi wengine wa ngazi ya taifa wa chama hicho.
Hata hivyo, Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hakusema maandamano na migomo hiyo itaanza lini, badala yake alitaka kila kiongozi wa wilaya kuwasilisha mkakati wa utekelezaji kwenye chama hicho taifa.
Viongozi wengine ambao vyama vyao vinaunda Ukawa waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi. Alisema anaitaka serikali na uongozi wa Bunge kuahirisha Bunge hilo haraka iwezekanavyo, vinginevyo wanachama wa Chadema wataingia mtaani kwa kuwa na maandamano yasiyo na ukomo.
“Tusifanywe wajinga. Maoni ya Watanzania yanachakachuliwa, fedha zinaliwa...natangaza azimio la mkutano mkuu ni kushirikisha umma kwa maandamano na migomo kwa kibali cha polisi na bila kibali...siko tayari kwa mazungumzo tena, nchi haiwezi kubadilika kwa mazungumzo ambayo ni kuchezea fedha za umma,” alisema Mbowe.
Alisema viongozi mbalimbali, wananchi na mashirika binafsi wameongea kutaka Bunge lisitishwe, lakini limeendelea kutumia fedha za umma bila huruma, huku wakijua hakuna Katiba itakayopatikana.
Mbowe, ambaye anatetea nafasi ya Mwenyekiti baada ya kumaliza muda wake, alisema yapo mazingira yanayolazimisha kuvunja sheria ili kupenyezwa ukweli, ambao ni kutumia maandamano na migomo isiyo na kikomo.
“Najua watatumia nguvu na kututisha na silaha za moto. Lakini sisi tutasonga mbele,” alisema.
Alitangaza maazimio matano ya mkutano mkuu, ambayo ni mtandao wa chama na wananchi kushirikiana na Ukawa kila wilaya kufanya maandamano na migomo hiyo.
Wanasheria wote wa Ukawa wakutane na kuona uwezekano wa kufungua kesi dhidi ya wajumbe wa Bunge hilo.
Lingine ni kuwashambulia kisiasa wajumbe wa Bunge hilo, ambao ni wabunge katika majimbo yao kwa kuhakikisha hawarejei tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Azimio lingine ni kwa Mkoa wa Dodoma kufanya maandamano kuelekea kwenye kumbi za vikao vya Bunge ili kuwafanya wajumbe wasiendelee na Bunge hilo kwa kuwa kinachoendelea ni wizi, matusi na ukatili wa dhahiri dhidi ya Watanzania.
“Nawaagiza wajumbe wote wa mkutano mkuu kuleta mipango ya utekelezaji wa maazimio haya haraka kwa ajili ya kuanza utekelezaji,” alisema.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema mipango mingine ya kimkakati itaendelea baina ya viongozi wa Ukawa.
Alisema nchi iko kwa ajili ya mabadiliko, lakini tatizo kubwa ni uoga wa Watanzania, hivyo ni wajibu wa viongozi hao kuwaimarisha wananchi kwa kuwajenga kifikra.
“Sitaki fujo na wala sikusudii nchi iingie kwenye fujo. Tunataka haki ya wananchi. Tumeongea sana. Haitoshi kwa sasa. Sipo tayari kuzungumza, bali kuchukua hatua…wanaoendelea na vikao na kujitajirisha na fedha haramu ni wizi, ukatili na ubatili kwa mwenyekiti kubadili rasimu, sheria na kanuni atakavyo,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Napenda serikali ya Chama Cha Mapinduzi itambue katiba bora haipatikani kwa kuamuliwa kupiga kura au wingi, bali kwa maridhiano…viongozi wa dini, asasi na wananchi wamesema, lakini mwenyekiti anacheza na kodi zetu,” alisema Mbowe.
Rushwa
Mbowe alisema kiongozi yeyote wa Chadema ambaye atakamatwa na rushwa, atachukuliwa hatua, ikiwamo kufukuzwa uanachama na kuwataka wanachama kuacha kufikiri kuwa ndani ya chama hicho ni mahali pa kutoka kimaisha.
Alisema wanachama na viongozi wengi wa chama hicho wanajitolea kwa kuwa wana kiu ya mabadiliko na rushwa siyo sehemu ya maisha yao ya kila siku, bali kujali maisha ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mbowe alisema ndani ya chama hicho hakuna ulaji, bali kufanya kazi kwa kujitolea zaidi na kwamba, chama hicho hakijiendeshi kwa kutegemea fedha za wahisani na hawajapewa fedha zozote kwa ajili ya mkutano huo.
HISTORIA YA CHADEMA
Mbowe alitumia mkutano huo kueleza historia ya chama hicho, huku akifananisha na treni inayokwenda Kigoma yenye vituo mbalimbali na katika kila kituo kutakuwa na abiria watakaoteremka na kupanda, huku wengine hawatateremka hadi wafike mwisho, ambako ni Ikulu.
“Jinsi chama kinavyozidi kukua, ndivyo kinavyozidi kushambuliwa…nia, uwezo na sababu tunayo. Hivyo, tunasonga mbele. Uzoefu wa miaka 23 umetosha. Sasa tunastahili kuingia Ikulu,” alisema.
“Hatutakubali msaliti kumuonea aibu. Hakuna mwenye sifa na umaarufu kuliko Chadema. Hiki ni chama kinachoundwa na damu, majeraha, uvumilivu na kujitoa kwa hali na mali kwa wanachama wake. Hivyo, hatutakubali kuvurugwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbowe, kazi ya chama cha siasa ni kujenga fikra za wananchi na siyo kujenga maofisi na kwamba baada ya uchaguzi wa chama, wataanza mafunzo kwa viongozi.
DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alitaka kuwekwa wazi kwa daftari la kudumu la wapigakura, ikiwa ni pamoja na wadau kushirikishwa kwa uwazi kuliko hali ilivyo sasa kwa chama kimoja kushirikishwa, huku vingine vikiachwa na kwamba hali iliyo itaondoa nchi kuingia kwenye machafuko.
Alitaka kuundwa kwa tume ya kimahakama kuchunguza vifo vya raia vilivyofanywa na polisi kwenye maeneo mbalimbali nchini, huku kukiwa na kesi nyingi zinazofunguliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho.
DK. LWAITAMA
Mwanazuoni Exaveri Lwaitama, alisema Ukawa haihitaji kusajiliwa, bali ni mapambano ya mabadiliko ambayo yapo kichwani mwa Watanzania.
Aliwataka kutoangalia mtu mmoja mmoja kupata uongozi, bali uwezo wa mtu bila kujali chama anachotoka.
PROFESA LIPUMBA
Profesa Lipumba alisema tunu za kusimamia uwajibikaji zimeainishwa kwenye rasimu ya Katiba na kwamba baada ya CCM kuisoma na kuona inawawajibisha, wameamua kuchakachua kwa kuondoa mambo muhimu.
Alisema Ukawa imejenga kuaminiana na kuaminika kwa maoni ya Watanzania na kwamba Bunge linaendelea, huku wakijua hawawezi kupata katiba kwa kuhalalisha uwapo wao Dodoma, huku wakiendelea na matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Lengo letu ni kufika mahali pa kufanya mkutano wa vyama vyote vya Ukawa na kupendekeza mgombea mmoja wa urais, tushirikiane. Vyama ni nyenzo katika kupata haki za raia kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa rasilimali zetu kutumika kwa manufaa ya wote,” alisema.
Alisema ni aibu kwa Tanzania kuwa na watoto wenye utapiamlo, kwani kati ya watoto 100, 42 wanakosa lishe bora na kina mama wakikosa huduma bora za afya.
MANGULA
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, alisema siasa siyo chuki, bali ni tofauti za kisera, kiitikadi na falsafa na kwamba utaratibu wa kukutana mara kwa mara utawaweka pamoja.
MBATIA
Mbatia alisema Ukawa ni nyezo ya kurekebisha makosa ya nyuma na sasa wanasonga mbele bila woga na ni vyema CCM ikatambua kuwa nchi ni ya wote na siyo mali yao.
Alivitaka vyama vya CCM, Chadema na CUF kuzungumza kwa kuhakikisha mama ambaye ni Tanzania, anapewa upendo na kunyonyesha mtoto wake akue vizuri na kuacha mifarakano na kutupiana maneno.
Alisema kuendelea kwa Bunge hilo kwa kupoteza fedha za umma ni lazima waonyeshe chuki ya wazi na Ukawa wataendelea kushirikiana na kuaminiana.
DK. MAKAIDI.
Dk. Makaidi alisema Ukawa ni ligi ya kuleta maendeleo Tanzania na wataogelea na kuzama pamoja kwa kuwa ndilo tumaini kwa Watanzania.
Alisema ndani ya Ukawa kuna wapiganaji mahiri wanaoweza kuleta mabadiliko chanya na ni vyema kila chama kikatoa maazimio juu ya suala la uchaguzi wa serikali za mitaa ambao haueleweki.
JAJI MUTUNGI.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, aliwapongeza Chadema kwa kudumisha demokrasia kwani chama kufanya mkutano mkuu ndiyo demokrasia.
Alisema hakwenda kwenye mkutano huo kama mtafiti au mchambuzi wa mkutano mkuu, bali kwa cheo chake.
TCD.
Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Daniel Loya, alisema demokrasia ndani ya vyama vya siasa ni tatizo kubwa na kufanya mkutano mkuu na kuchagua viongozi ni hatua kubwa ya kidemokrasia.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na baadhi ya Mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wa dini, taasisi, wabunge wa chama cha ODM Kenya, vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa.
Wakati wa utambulisho, Dk. Slaa aliwatambulisha viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa kama ndugu wa damu na kusema ushirikiano wao ni wa kudumu.