Wanawake na watoto waliokuwa wakishikiliwa mateka na kikundi cha Kiislam cha Boko Haram kaskazini mwa Nigeria wamesema baadhi yao waliuawa kwa kupigwa mawe na wapiganaji wa Boko Haram wakati jeshi lilipokaribia kuwaokoa.
Walikuwa wakizungumza siku moja baada ya karibu mateka mia tatu kuokolewa kutoka msitu wa Sambisa na kuwapeleka katika kambi ya serikali.
Mwanamke mmoja ambaye alijifungua akiwa mateka ameelezea namna wapiganaji hao walivyomkata koo mumewe wake mbele yake, kabla mwanamke huyo kutenganishwa na watoto wake wengine watatu.
Mwandishi wa Associated Press ambaye aliotembelea kambi hiyo amesema wengi wa watoto waliokolewa walikuwa wanaugua utapiamlo mkali.
Jeshi la Nigeria limesema limewaokoa zaidi ya watu mia saba katika kipindi cha wiki moja iliyopita wakati wa mapigano makali yanayoendelea dhidi ya Boko Haram.