Waziri wa Kazi na Ajira Mhe. Gaudensia Kabaka amesoma Muswada wa Sheria
ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini wa mwaka 2014 kwa mara ya pili ikiwa
muswada huu umelenga masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi
pamoja na mahitaji ya kiteknolojia ambayo ni kichocheo kikubwa cha
uhamiaji wa nguvu kazi kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Mhe.Kabaka alisema kwa sasa zipo mamlaka nyingi zinazotoa vibali vya
ajira kwa wageni kwa kuzingatia sheria zinazosimamia maswala ya
Uhamiaji, Uwekezaji, Elimu, Biashara na Wakimbizi, hivyo hali hii ya
kuwepo na mamlaka nyingi zinachangia kusababisha usumbufu kwa
wawekezaji na kokosekana kwa uwajibikaji pamoja na kuwepo na
udanganyifu.
“Kutungwa kwa sheria hii kunalenga kutelekeza kwa manufaa ya nchi yetu
mikataba ya kikanda inayoruhusu uhamiaji huru wa nguvu kazi hususani
inayohusu itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afika Mashariki na
Ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika SADC” alisema Mhe.
Kabaka.
Katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uhamiaji na
nguvu kazi, utaratibu wa kutoa vibali vya ajira kwa wageni umekuwa
ukitumika ili kuhakikisha nguvu kazi ya wageni hao inaleta manufaa kwa
maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na pia katika kulinda ajira za
wananchi.
Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Mhe.Celina Paresso
Mbuge wa Viti Maalum-CHADEMA aliishauri Wizara ya Kazi na Ajira
kushirikiana na wizara mtambuka kama Wizara ya Viwanda na Biashara na
Idara ya Uhamiaji, kufanya ukaguzi wa vibali vya ajira hasa katika
maeneo ambayo raia wa kigeni wanafanya shughuri zao bila kuzingatia
sheria za nchi.
“Tanzania tuna maliasili nyingi, lakini dunia ya leo na ijayo
itatawaliwa na wenye maarifa, kwa maana ya sayansi, teknolojia, elimu na
ujuzi” alisema Mhe. Paresso
“kuwa na maliasili peke yake haitoshi, hatuna budi tujinoe kwa elimu na
ujuzi, na hasa elimu inayomuwezesha mtu aajirike au ajiajiri” aliongezea
Mhe. Paresso
Endapo Mhe. Rais ataridhia, Sheria hii itaanza kutumika tarehe 1 Julai,
2015. Kutungwa na kuanza kutumika kwa Sheria ya Ajira ya Wageni Nchini
kutakuwa na matokea chanya ikiwema uratibu mzuri wa ajira za wageni
nchini, kuongezeka kwa ajira za watanzania na kuongezeka kwa ujuzi kwa
wafanyakazi wa Tanzania.