Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais
Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji
mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba
yeye ndiye anawatuma.
Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo jana, Gwajima alisema amekuwa
akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani yeye si raia wakati ni
Mtanzania halisi.
“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa… asipowakemea, basi
kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma,” alisema Gwajima
huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.
Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa wakimsikiliza Askofu
Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa kwa mara ya pili na
polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana na usajili wa
kanisa, uongozi na mali zake.
Uraia wake
“Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani
mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa,” alisema.
Alisema makundi ya jamii yamekuwa yakitoa kauli mbalimbali lakini hayabughudhiwi anavyofanyiwa.
“Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao
lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu
kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana,” alisema.
Kuhusu utajiri wake
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya Serikali vinavyohoji
utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya waumini. Alisema
anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake
na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.
“Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe
Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata
wapi?” alisema na kisha kuwauliza waumini hao… “Hivi baba yenu
nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?”
Alijibiwa, “Tutakupaaaa!” Baada ya majibu hayo waumini hao walianza
kupeleka fedha katika jukwaa kuu huku wakiimba nyimbo za kumtukuza
Mungu.