Siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu (Nec)
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kusema Mbunge wa Monduli,
Edward Lowassa, anaweza kupoteza sifa za kuwania urais kutokana na
makundi ya jamii yanayomiminika nyumbani kwake kumshawishi awanie nafasi
hiyo, Lowassa amemjibu na kusema hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono.
Kadhalika, Lowassa amesema mambo ya Chama hayajadiliwi mtaani (kwenye
vyombo vya habari), bali malalamiko yoyote yanapelekwa kwenye vikao
halali vya CCM, yanajadiliwa na kutolewa uamuzi kwa mujibu wa kanuni na
taratibu.
Hata hivyo, amewataka wafuasi wake pamoja na makundi mbalimbali ambayo
yalikuwa yamejiandaa kwenda nyumbani kwake kumshawishi, wasitishe kwanza
safari yao hadi hapo Chama kitakapotoa maelekezo ya ‘namna ya
kushawishi.’
Lowassa aliyasema hayo nyumbani kwake jana, alipokuwa akipokea ujumbe wa
waendesha bodaboda 60 kutoka Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya ambao
walikwenda kumshawishi awanie urais muda utakapofika.
Alisema kwa kanuni na taratibu za CCM, mambo ya chama humalizwa kwenye
vikao vya chama, kwa kuzungumza hadi kuelewana na kufikia muafaka,
lakini siyo kwenye vyombo vya habari.
“Mambo ya Chama hayawezi kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari kwenye tv,
redio; mara huyu hivi, huyu hivi, mkiona chama kinakwenda kwenye
utaratibu huo ni hatari sana…CCM ninayoijua mimi ni ya vikao, kwa hiyo
sikusudii kujibu hizo hoja, kwanza rafiki yangu Bashe (Hussein),
amezieleza vizuri sana, lakini sikusudii kusema zaidi ya hayo
yaliyosemwa na Bashe,” alisema.
Alisema anashangaa kuona watu wakizusha kwamba watu wanaokuja nyumbani
kwake kumshawishi amewaita na kuwalipa jambo ambalo ni uongo kwa kuwa
hana fedha za kulipa watu wengi wanaokuja kwake na hana pia uwezo wa
kuwapikia chakula.
“Wanasema mnakuja nimewaiteni ninawapa fedha, hela za kuwapa ninazitoa
wapi, mkija hapa nikiwawekea maturubai ni kosa, mkiwa na viti ni makosa
na wanasema nawapikieni chakula. Mambo ya ajabu sana, yanasemwa na watu
wazima watu wenye heshima zao; juzi kulikuwa na vijana 300 hapa,
nitawapikia chakula nitaweza wapi, ni vibaya sana kumdhalilisha mwenzako
kwamba maisha yake yote akili yake ni kufikiria tumbo, huyu hana cha
kufikiri isipokuwa tumbo,” alisema Lowassa.
“Nimewahi kuja huko Mbarali kuwashawishi mje kwangu? Au nimewapeni
hela leo mlipokuja hapa, hata soda zenyewe hamjanywa,” alisema
Lowassa huku vijana wakisema hawajashawishiwa naye.
Aliongeza: “Yananisikitisha sana maneno hayo, lakini hayanikatishi tamaa
nitaendelea kama ilivyo kawaida. Nawahakikishie nimeyasikia maneno
hayo, lakini najua maneno mazuri huwa yanazungumzwa kwenye chama,
nategemea yatajadiliwa kwenye vikao vya chama.”
Lowassa alisema: “Na utaratibu huu ulioanza na watu, (kuja nyumbani
kwake), mimi ni vigumu kuuzuia. Mimi ni vigumu kuzuia mafuriko kwa
mikono. Mafuriko yanakuja mimi nayazuia kwa mikono, nitaweza kweli?”
“Ila nashauri tufanye hivi, wengine ambao hawajaja wanisikilize, hebu
tusubiri Chama kitoe maelekezo, kama wamesema hii inatafsiriwa kwamba ni
kampeni, tungoje basi wasema tufanye nini watu wanaotaka kuja
kushawishi,” alisema.
Alisema watu wanaokwenda kumshawishi wanatii maelekezo yaliyotolewa na
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ambayo aliyatoa mjini
Songea wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM, aliposema kwamba wanachama
wanaweza kumshawishi mgombea wanayeona anafaa.
“Na mimi nilikuwapo kiwanjani pale akasema mkiona hao waliopo hawatoshi,
bado muda upo washawishini wengine waingie. Sasa mkifanya hivi ni kosa,
ni kampeni, ipi ni kampeni na ipi siyo kampeni?,” alisema na kuhoji.
“Kwa hiyo nawashauri wale ambao hawajaja, tusiingize mgogoro kwenye
Chama, tungoje tupate maelekezo, mimi ninahakika tutapata nafasi, jambo
moja ninahakika na ninataka kuwapa matumaini ipo siku Watanzania
watapata uhuru wa kusema juu ya mtu mimi, iko siku watapiga kura zao
kusema naam ama hapana kwa hiyo tungojee hiyo siku.”
Alisema anatambua Watanzania wengi wanampenda kwa kazi zake alizofanya
akiwa kwenye ngazi mbalimbali serikalini na kutaka wanaomshambulia
wasubiri Watanzania wenyewe waamue kwenye sanduku la kura.
“Ninahakika wapo Watanzania wengi wanaonipenda kama walivyosema kwa kazi
zangu, watapata nafasi ya kusema naam ama hapana, kwa hiyo huyo
anayepiga kelele nyingi sijui nitoke kwenye chama sijui nifanye kitu
gani angoje wanaCCM na Watanzania waamue. Mimi ni mwanademokrasia
naamini kwenye demokrasi, lakini naamini kwenye utendaji bora, kama
mlioufanya leo wa kutembea kilometa 600 kutoka Mbarali kuja kunitembelea
hapa ni kazi kubwa ya utashi mkubwa sana, ni watu wanaojitolea,
wanaojiamini, na mimi ninaamini Watanzania wengi wanaoniamini kwa mambo
ambayo nimeyafanya,” alisema.
Aliwasihi vijana hao kupuuza taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya
habari jana na kuwaomba waendelee kukiunga mkono chama hicho.
Alisema safari ya vijana hao kusafiri kilimita 600 kwa bodaboda kutoka
Mbarali imemtia moyo na haya kwa kuweka wazi mambo wanayoyaamini.
Alisema vijana wa bodaboda wanafanya kazi kubwa nchini ikiwamo ulinzi na
usalama hivyo ni kundi linalohitaji kuendelea kusaidiwa.
“Mimi nitaendelea kushirikiana nao siku zote katika nafasi yoyote
nitakayokuwa nayo. Mmekuja siku mbaya kidogo kwa sababu jana kuna watu
wamesema kwenye vyombo vya habari maneno mengi ambayo kwa malezi yangu
mimi mambo ya chama humalizwa kwenye vikao siyo kwenye vyombo vya
habari, lakini yasiwakatishe tama,” alisema.
Awali, Kamanda wa Vijana wa CCM wilayani Mbarali, Ibrahim Mwakabwanga,
alisema Lowassa hana uwezo wa kushawishi kila kundi na hata wao
wamejikusanya wenyewe, wamejigharimia na wameacha shughuli zao na kuamua
kuja Dodoma kumshawishi kwa kuwa wanaona ndiye kiongozi ndani ya CCM
anayefaa kwa sasa.