Goli
la kwanza la Mario Balotelli kwenye michuano ya ligi kuu England
limeipa Liverpool ushindi muhimu dhidi ya Tottenham Hospurs katika dimba
la Anfield kuwania nafasi nne za juu za msimamo wa ligi hiyo.
Lazar Markovic aliipa Liverpool bao la mapema la kuongoza bao ambalo lilirudishwa na Harry Kane wa Tottenham...>>>>Bao la Steven Gerrard baada ya mapumziko lilifanya Liverpool kuongoza tena mchezo huo lakini Mousa Dembele alisawazisha tena kabla ya Mario Balotelli kuzifuma nyavu na kuifanya liverpool kuondoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao matatu kwa mawili.
Katika Mchezo mwingine, Arsenal imepanda mpaka kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi kuu ya England baada ya kuifunga Leiceter City magoli mawili kwa moja.
Atashukuriwa sana Mesut Ozil aliyetengeneza mipira kwa Laurent Koscielny na Theo Walcott, mipira ambayo ilizaa magoli hayo mawili na kunyakua nafasi ya nne iliyokuwa ikishikiliwa na Mancheater United.
Goli moja la Leiceter lilifungwa na Andrej Kramaric.
Katika mchezo mwingine QPR iliichapa Sunderland magoli mawili bila majibu na Mchezo kati ya Hull City na Aston Villa ulimalizika kwa Hull city kutoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Aston Villa.